Saturday, September 17, 2011

Vijana washtukia mtego wa CCM

VIJANA wanaharakati wa mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wameonyesha kushtushwa na mkakati wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 sasa kwa kuwarubuni vijana kwa kuanzisha Benki ya Vijana nchini.
Walidai kuwa kuanzishwa kwa benki hiyo si suluhisho la tatizo la ajira kwa vijana nchini, kutokana na mfumo wa uanzishwaji wake ulivyo kwa sasa ambao una lengo la kuwavuta vijana kisiasa zaidi.
Wakizungumza katika kipindi cha malumbano ya hoja kilichorushwa na kituo cha televisheni cha juzi, walisema wazo la kuwa na benki ya vijana ni zuri na linaungwa mkono na vijana wote, ila mfumo wa uanzishwaji wake ndio unawatia hofu.
Walisema kutokana na hali ya kisiasa ilivyo na vijana wengi kupoteza imani na CCM, ni wazi chama hicho kimekuja na wazo hilo la kuanzisha benki kama njia ya kujijenga kisiasa.
Ally Salum Ally kutoka Pemba alisema kuwa benki hiyo ilipaswa kuanzishwa baada ya kuunda chombo cha vijana ambacho kitakuwa huru pasipo kufungamana na chama chochote cha kisiasa.
Sarah Kyando kutoka mkoa wa Mbeya alisema kuwa serikali ya CCM imeendelea kuja na mikakati mbalimbali ambayo mwisho wa siku imejikuta ikizidi kuchafuka zaidi kutokana kutokuwa na utekelezaji.
Mwakilishi wa benki hiyo, Christopher Ngubiagai, akijibu maswali ya wanaharakati hao alisema kuwa benki hiyo pamoja na kuanzishwa na UVCCM, haitabagua vijana wa vyama vingine.

Source Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

hostgator coupon code