Tanzania itafaidika na msaada wa Euro Milioni 15 ( zaidi ya Sh30 bilioni ) toka Serikali ya Uholanzi kugharimia mradi wa Kujenga Uwezo kwa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini, unaojulikana kwa jina la Netherlands Initiative for Capacity Development in Higher Education(Niche). Hayo yalibainishwa na meneja wa mradi huo, Ute Jansen, alipotembelea Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa chuo kikuu hicho, mradi huo unatoa ufadhili kwa Shule ya Biashara na kuboresha mafunzo ya utawala wa Serikali za Mitaa. Jansen, alisema ana matumaini makubwa sana kuwa mradi huu utakapokamilika, utaboresha sana zile sekta zilizoainishwa kwenye mradi huu ambazo ni kujenga uwezo katika kutoa elimu kuhusu afya, sekta binafsi na Serikali za Mitaa. Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo Tanzania, kupitia Shirika la NUFFIC, Johanna Van Nieuwenhuizen, alisema Uholanzi imeridhishwa na jinsi Tanzania inavyoitumia misaada toka nchini mwake, hivyo kujihakikishia fursa zaidi za kusaidiwa katika miradi mbalimbali. Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Mugishi Mgasa, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, aliishukuru Serikali ya Uholanzi kwa kufadhili mradi huo na kueleza kuwa ufadhili huo una maana kubwa sana kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe, kwa sababu utapanua uwezo wa chuo hicho katika kutoa Mafunzo ya Biashara na Utawala wa Serikali za Mitaa. Naye Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Joseph Kimeme, alisema ufadhili huo, utawafanya wanafunzi wanaomaliza Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, sio tu kuhitimu kwa elimu yenye ubora wa hali ya juu, bali pia watajengewa uwezo wa kujiajiri kwenye biashara zao kufuatia mahitaji ya soko. |
Thursday, September 22, 2011
Uholanzi yatoa Sh30 bilioni kugharamia elimu nchini
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment