Saturday, September 17, 2011

Serikali yasema "DC amedhalilishwa"....

SERIKALI imesikitishwa na udhalilishaji uliofanywa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Fatma Kimario juzi.

Imesema kwa kuwa nchi inafuata utawala wa sheria, inaviachia vyombo vya Dola vifanye uchunguzi wake.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, alipozungumza na gazeti hili akiwa Newala mkoani
Mtwara.

“Serikali imesikitishwa na udhalilishaji uliofanywa kwa DC wa Igunga. Nchi ina taratibu, kanuni na sheria kwa hiyo unaviachia vyombo vya Dola kufanya kazi yake. “Lakini tumesikitishwa na tukio lile kwa sababu DC alikuwa tayari kusema nao, alikuwa eneo lake la utawala akifanya kazi. Kwa nini wamkamate na kumtoa nje kwa udhalilishaji ule,” alisema Mkuchika.

Alisema haikuwa vyema kwa wahusika kufanya udhalilishaji huo hasa baada ya Mkuu huyo wa wilaya kuwa tayari kuzungumza nao; hivyo wangeweza kuzungumza naye ofisini katika mazingira ya ustaarabu.

DC Kimario alifanyiwa vurugu na vijana wa Chadema juzi akiwa katika shughuli zake za kikazi.

Vijana hao walidai DC alikuwa akifanya kampeni za kisiasa katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Igunga utakaofanyika Oktoba 2, mwaka huu.

Katika taarifa yake jana, Polisi ilisema DC huyo amefanyiwa shambulio la kudhalilisha kinyume cha maadili, ikiwemo kuvuliwa vazi lake la hijab ambalo humsitiri mwanamke wa Kiislamu hasa kichwani. Akizungumza jana wilayani Igunga, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Polisi, Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu, alisema mbali na kuvuliwa hijab, pia DC alidai alivuliwa viatu na kukatiwa mkufu.

"Pia simu yake ya mkononi aina ya Samsung ilipotea na alitukanwa matusi ya nguoni ya kumdhalilisha …(hatuwezi kuyaandika hapa)," alisema Mngulu akielezea madai hayo ya DC Kimario.

Alisema wakati Mkuu huyo wa Wilaya akifanyiwa vitendo hivyo na vijana hao wa Chadema, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Igunga, Sunera Manoti, alikwenda Polisi kutoa taarifa.

Hata hivyo, baada ya Polisi kupata taarifa hiyo, kwa mujibu wa Mngulu, walikwenda eneo la tukio na kukuta hali ni shwari na kuanza upelelezi baada ya majalada ya tuhuma; la kwanza la DC akilalamika kufanyiwa shambulio la aibu na la pili la Chadema wakilalamikia kuingiliwa katika mkutano wa kampeni.

Kwa mujibu wa taarifa za Chadema, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga, Mbunge wa Maswa Mashariki, Kasulumba Sylvester pamoja na shabiki wao ambaye jina lake halikupatikana waliitwa Polisi na kuhojiwa saa moja na kuachiwa kwa dhamana.

Madai ya Chadema Awali, kabla ya Polisi kuzungumzia hilo, Chadema iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuelezea makosa 15 ya DC huyo, likiwemo la kuitisha mkutano waliodai kuwa ni wa hadhara na kinyume cha sheria.

Akifafanua madai hayo, Mkurugenzi wa Chadema wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Singo, alidai kuwa mtu ye yote akitaka kufanya mkutano, lazima atoe taarifa kwa Polisi na kwa kuwa polisi walikuwa wakifahamu kuwepo kwa mkutano wa Chadema, wasingemruhusu DC kufanya wa kwake.

Hata hivyo, Mngulu alisema DC Kimario alikuwa katika kikao cha ndani na sio mkutano wa hadhara kama Chadema walivyodai, ambacho kisingehitilafiana na mkutano huo wa Chadema, lakini hata muda wa tukio la kushambuliwa Mkuu huyo wa Wilaya na mkutano wa Chadema vilikuwa tofauti.
  for more detail visit http://www.habarileo.co.tz/

No comments:

Post a Comment

hostgator coupon code