Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Magavana wa Afrika (ACBF) Dkt .Frannie Leautier(katikati)
akiongea na waandishi wa habari leo mjini Arusha kuhusu kuanza kwa Mkutano wa 20
wa Bodi ya Magavana wa Afrika(ACBF) unaotarajiwa kufunguliwa na Rais wa Tanzania
Jakaya Mrisho Kikwete siku ya Alhamis (8.9.2011). Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano(ACBF) Audrey Mpunzwana na kushoto ni Mtaalamu kutoka ACBF George
Kararach.Picha na Tiganya
Vincent-MAELEZO-Arusha
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa
Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa ACBF unaokwenda sanjari na mkutano wa tano
wa viongozi waandamizi utakaojadili jinsi ya kujenga uwezo kwa nchi wanachama
zitakazoshiriki. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 07- 09 Septemba, 2011
katika Hoteli ya Mount Meru mjini Arusha.
Mkutano wa Magavana wa ACBF utafunguliwa na
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzana Dkt Jakaya Mrisho Kikwete siku ya
Alhamisi tarehe 8 Septemba 2011 mjini Arusha.
Mkutano utawashirikisha Mawaziri, washirika
wa maendeleo na wadau wengine maarufu watakaojadili jinsi ya usimamizi mzuri wa
misaada na mikopo barani Afrika na namna wanavyoweza kukabiliana na changamoto
za ajira kwa vijana.
Mkutano wa Tano wa viongozi waandamizi
utatangulia mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa ACBF ambao utaongozwa na Waziri
wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mustafa Haidi
Mkulo.
Washiriki wa Mkutano wa Bodi ya Magavana wa
ACBF ni Mawaziri wa Fedha, wahisani kutoka nchi wanachama wa Bodi ya
Magavana(ACBF), viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia(WB), Benki ya
Maendeleo ya Afrika(ADB) pamoja na Programu za Maendeleo zinazosimamiwa na Umoja
wa Mataifa.
Katika mkutano wa tano wa viongozi
waandamizi, wasemaji wakuu wanatarajiwa kuwa Katibu Mtendaji wa ACBF Dkt.
Frannie Leautier, Waziri wa maendeleo ya Uchumi, Mipango na Uchambuzi wa Sera
Mh. Marcel De Souza kutoka Benin na Waziri Mkuu Mstaafu wa Mauritania Mh. Zeine
Ould Zeidane ambao wataongoza mjadala juu ya changamoto za ajira kwa vijana
barani Afrika na hatua gani zichukuliwe ili kukabiliana na changamoto
hizo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo Afrika
(Africa Development Institute) Bw. Victor Murinde kwa kushirikiana na Mkurugenzi
wa Sera za Uchumi (SEP) Bi. Sue Szabo, Mshauri wa Utawala bora wa Benki ya Dunia
Bw. Deryck Brown pamoja na Bw. George Kararach ambaye ni mtaalamu wa ACBF;
wataongoza majadiliano kuhusu taarifa ya viashiria vya uwezo wa Afrika kuelekea
mkutano wa Busan, Korea ya Kusini mwezi Novemba, 2011utakaojadili uratibu,
usimamizi na ufanisi wa misaada.
Mojawapo ya mada itakayojadiliwa katika
mkutano wa viongozi waandamizi hao ni pamoja na hoja ya kujenga uwezo kwa nchi
za Bara la Afrika.
ACBF ni mdau muhimu katika kuimarisha
ushirikiano na bara la Afrika ikiwemo Umoja wa Afrika(AU) pamoja na Shirika la
Maendeleo la Afrika(NEPAD).
Madhumuni ya ACBF na washirika wa
maendeleo, ni kuimarisha nafasi ya Afrika na kuonyesha umuhimu wa kutambua sauti
ya Nchi zinazoendelea katika kujenga uwezo.
Vilevile, katika kipindi cha miaka miwili
iliyopita ACBF imejiunga na masharika kama vile Taasisi ya Uchumi na Maendeleo
ya Jumuiya ya Ulaya (OECD), Mtandao wa Mafunzo ya Kujenga Uwezo (LenCD),
Wanaharakati wa Masuala ya Siasa wa Nchi za Kusini, Ushirika wa CD (CD Alliance)
ambao hufanya kazi kwa pamoja kwa kuainisha vipaumbe na mada kuhusu kujenga
uwezo kwa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini
Arusha, Katibu Mkuu wa ACBF Dkt Frannie Leautier alisema kuwa lengo la mkutano
huo ni kujadiliana na kubadilishana taarifa, maarifa, utalaam na uzoefu kuhusu
namna ya uratibu na usimamizi mzuri wa misaada. Alisema kuwa mkutano huo
utasaidia kuboresha ubunifu na utekelezaji wa sera zitakazosaidia kupata matokeo
endelevu.
Dkt. Leautier alisema kuwa hatua ya
kuwaleta pamoja wataalam mbalimbali wanaohusika na uratibu na usimamizi wa
misaada ya wahisani itawasaidia washiriki kujifunza mambo mbalimbali na kupanua
uelewa wa wadau katika eneo hilo kwa lengo la kutaka kuimarisha uwezo wa Afrika
na pia kutoa fedha pale panapohitajika.Aliongeza kuwa mifumo
ya utendaji wa wahisani inapaswa kuendana na kanuni ya uendelezaji na kujenga
uwezo.
No comments:
Post a Comment