Friday, September 16, 2011

wabunge chadema wakamatwa kwa tuhuma za kumvamia mkuu wa wilaya

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Susan Kiwanga (Viti Maalum) na Sylivester Kasulumbai (Maswa Mashariki), wamehojiwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tabora wakituhumiwa kushiriki kumvamia na kumpiga Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Fatma Kimario.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Igunga, jana, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Makao Makuu ya Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Mungulu, alisema wabunge hao walikamatwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa.
Akizungumzia kile kilichotokea, Mngulu alisema mkuu huyo wa wilaya alikwenda katika kijiji cha Isakamaliwa kufanya mkutano wa ndani na watendaji wa kijiji hali iliyowafanya wafuasi na viongozi wa CHADEMA kuchukizwa kwa madai kuwa wameingiliwa.
“Mkutano wa CHADEMA katika kijiji cha Isakamaliwa ulikuwa ufanyike kati ya saa nne na saa sita. Kikao cha mkuu wa wilaya kilifanyika kati ya saa 7:30 na saa 9:00 alasiri muda ambao CHADEMA hawakuwa na mkutano,” alisema.
Hata hivyo, kamanda huyo wa polisi alikiri kuwepo kwa malalamiko ya CHADEMA kuhusiana na kuingiliwa katika maeneo waliyotengewa kufanya kampeni na ukiukwaji wa maadili unaodaiwa kufanywa na mkuu huyo wa wilaya lakini akadai msemaji wa mambo hayo ni msimamizi wa maadili ambaye ni mkurugenzi wa uchaguzi.
Aidha alikiri kwamba askari wake walikuta hali ya amani na utulivu katika kijiji hicho, ndipo walipolazimika kuanza upelelezi kujua ukweli wa tukio hilo.
Aliongeza kuwa tuhuma zinazochunguzwa dhidi ya wabunge hao na wafuasi wengine watatu wa CHADEMA, ni kuvamia kikao cha mkuu wa wilaya.
Taarifa hizo zinadai kwamba katika tukio hilo mkuu wa wilaya alivuliwa hijabu, viatu, kukatiwa mkufu ambao thamani yake haijajulikana.
“Anadai kuwa simu yake ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya sh 400,000 ilipotea na kumtukana matusi ya nguoni,” alisema na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa Ofisa Tawala wa Wilaya, Sumera Manoti.
Taarifa zimebainisha kuwa mkuu huyo wa wilaya amefungua jalada la shambulio la aibu namba IR/1115/2011, wakati CHADEMA wamefungua jalada namba IR/1115/2011 linalohusu kuingilia mkutano wa kampeni kwa mujibu wa ratiba ya msimamizi wa uchaguzi. Kwa sasa jeshi hilo linaendelea kukusanya ushahidi kuhusiana na kesi hizo.
Hata hivyo, Kamanda Mngulu alitoa wito kwa vyama, viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi hususan kipindi hiki cha uchaguzi.
Juzi mkuu wa wilaya hiyo akiwa katika kijiji cha Isakamaliwa, tarafa ya Igunga alivamiwa na viongozi, wafuasi na mashabiki wa CHADEMA muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha ndani na watendaji wa vijiji.
Mbowe, Dk Slaa kuzunguka nchi nzima
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuanzia sasa yeye na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, watazunguka nchi nzima kuwahamasisha watu waikatae CCM na kuichagua CHADEMA.
Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Sikongo, mkoani Tabora, alipofanya mikutano ya hadhara pamoja na kuzindua kampeni za udiwani wa kata ya Kisanga.
Dk. Slaa alisema binafsi ameamua kuacha kukaa ofisini baada ya kutembelea maeneo mengi ya nchi na kuona watu wanavyoishi kwa umaskini ilhali wamezungukwa na rasilimali lukuki.
“Moto tunaouwasha sasa CCM hawajawahi kuuona. Sitakaa ofisini mpaka kieleweke, taifa linahitaji ukombozi na sisi tuko tayari kuwakomboa wananchi,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa Watanzania wako katika hali mbaya kwa sababu CCM imeshindwa kuzitumia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya walio wengi.
Alisema umaskini unaowakabili wananchi hivi sasa si laana kutoka kwa Mungu bali ni maamuzi mabovu ya wananchi kuwachagua viongozi wenye kuweka mbele ulaji na maslahi binafsi.
“Tumebarikiwa rasilimali lukuki lakini wananchi tunapumulia mashine kwa umaskini, watu wetu wanaishi kwenye nyumba za tembe, hawajui bati wala umeme, hili halikubaliki hata kidogo,” alisema.
Dk. Slaa alisema kama Watanzania wanataka ukombozi ni lazima waache woga wa kuwachagua viongozi wa CCM ambao hawana uchungu wa matatizo ya wananchi.
Naye mgombea udiwani wa kata ya Kisanga, Mgombozi Ntewi (CHADEMA), alisema mabadiliko ya kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa hayawezi kufanyika kama wananchi wataendelea kuwa waoga.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo atahakikisha michango yote inayotolewa na wananchi inatumika kwa kazi zinazotakiwa.
“Maendeleo makubwa tutayapata iwapo mtanichagua kuwa diwani wenu; viongozi wetu wanatafuna fedha za miradi kwa manufaa yao, mimi nitawabana vilivyo,” alisema.

No comments:

Post a Comment

hostgator coupon code